Proverbs 9

Makaribisho Ya Hekima Na Ya Upumbavu


1 aHekima amejenga nyumba yake;
amechonga nguzo zake saba.

2 bAmeandaa nyama na kuchanganya divai yake;
pia ameandaa meza yake.

3 cAmewatuma watumishi wake wa kike, naye huita
kutoka mahali pa juu sana pa mji.

4 dAnawaambia wale wasio na akili,
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa!

5 eNjooni, mle chakula changu
na mnywe divai niliyoichanganya.

6 fAcheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi;
tembeeni katika njia ya ufahamu.


7 g“Yeyote anayemkosoa mwenye mzaha
hukaribisha matukano;
yeyote anayekemea mtu mwovu
hupatwa na matusi.

8 Usimkemee mwenye mzaha la sivyo atakuchukia;
mkemee mwenye hekima naye atakupenda.

9 hMfundishe mtu mwenye hekima
naye atakuwa na hekima zaidi;
mfundishe mtu mwadilifu
naye atazidi kufundishika.


10 i“Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,
na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.

11 jKwa maana kwa msaada wangu
siku zako zitakuwa nyingi,
na miaka itaongezwa katika maisha yako.

12 kKama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo;
kama wewe ni mtu wa mzaha,
wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”


13 lMwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele;
hana adabu na hana maarifa.

14 mHuketi kwenye mlango wa nyumba yake,
juu ya kiti katika mahali pa juu sana pa mji,

15 nakiita wale wapitao karibu,
waendao moja kwa moja kwenye njia yao.

16 oAnawaambia wale wasio na akili,
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!”

17 p“Maji yaliyoibiwa ni matamu;
chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”

18 qLakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo,
kwamba wageni wake huyo mwanamke
wako katika vilindi vya kuzimu.
Copyright information for SwhKC